Monday, September 30, 2013

MNYIKA AMTAKA JK KUITISHA MKUTANO KERO YA MAJI.


MH. JOHN MNYIKA MBUNGE WA UBUNGO.


MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuitisha mkutano wa wadau haraka, ili kuzungumzia tatizo la maji kama alivyoahidi katika ziara yake ya Machi mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Mnyika alitoa ombi hilo ili kusitisha mchakato wa kukusanya maoni ya wadau unaofanywa na Mamlaka ya Huduma za Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) wa kutaka ongezeko la bei ya maji, kuwezesha Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salam (Dawasa na Dawasco) kufanya matengenezo ya lazima ya miundombinu.

Dawasa na Dawasco zilipeleka mapendekezo Ewura ya kutaka bei mpya kulipia maji safi kwa lita 1,000 iwe sh 1,627 badala ya sh 1,071 ya sasa na majitaka kutaka yalipiwe sh 302 kwa lita 1,000 badala ya sh 275.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mnyika alisema hizo ni gharama kubwa zisizo za msingi ambazo zimelengwa na Dawasa na Dawasco kuwatwisha mzigo wananchi wachache wanaopatiwa huduma ya maji huku wengi wao wakiwa hawana huduma.

“Baada ya kuziondoa au kuzipunguza bei hizo ambazo ninazipigia kelele kila siku huku nikitaka huduma iongezwe, wao wanataka kuziongeza. Huko ni kuwanyanyasa wananchi ambao hawana pa kukimbilia.

“Ongezeko la bei ya maji linalofanywa sasa na Dawasa na Dawasco ni kielelezo kwamba kuna ufisadi mkubwa unaofanywa na mamlaka hiyo ambayo imeshindwa kueneza huduma ya maji na kudai madeni ya serikali badala yake inataka kuwaonea wananchi,” alisema Mnyika.

Alisema ufisadi wa Dawasa na Dawasco umeonyeshwa katika ripoti za hivi karibuni za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambao hasa unafanywa katika mikataba, na kumtaka CAG aiweke wazi tena.
Kuthibitisha ukubwa wa tatizo hilo, Mnyika alitoa mfano kwamba Dar es Salaam na wakazi zaidi ya milioni 4 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, lakini wanaopata huduma ya maji si chini ya wananchi 100,000.

No comments:

Post a Comment