SERIKALI imewahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwa wingi
katika maeneo ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA)
kwa faida yao na ya nchi kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene, alisema uwekezaji
katika maeneo hayo una uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa
masoko ya nje na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa haraka.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki
alipotembelea Kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Co. LTD kilichopo eneo
la EPZA.
“Maeneo haya yana fursa nyingi ambazo wawekezaji wanaweza kufaidika
nazo…nawahamasisha waje kwa wingi na serikali itawasaidia kuweka
mazingira bora zaidi,” alisema Mbene.
Kiwanda hicho kinatengeneza nguo kwa ajili ya soko la nje ya nchi.
“Nina furahi kuona kiwanda hiki kimetoa ajira kwa Watanzania
wengi…haya ndiyo mambo ambayo serikali inapigania wakati wote,” alisema.
Kabla ya kufanya ziara katika kiwanda hicho, naibu waziri huyo alikutana na watendaji wa EPZA na kufanya nao mazungumzo.
Katika mazungumzo yao, aliwahakikishia watendaji na viongozi wa
mamlaka hiyo kuwa serikali itaendelea kushirikiana nayo katika kusukuma
gurudumu la maendeleo.
Meneja Mkuu Msaidizi wa Tanzania Tooku Garments Co Ltd, Rigobert
Massawe, alisema kiwanda hicho kinazalisha nguo aina ya jeans na tisheti
kwa ajili ya masoko ya nje.
Alisema kwa sasa wanatumia zaidi soko la Marekani na baada ya maboresho zaidi watauza katika soko la Uingereza.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, kiwanda kimeajiri Watanzania zaidi ya 800
na kinatarajia kufikia mwaka 2025 kitaweza kuajiri watu 15,000.
Akizungumza hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk.
Adelhelm Meru, alisema mamlaka yake imedhamiria kuona uwekezaji unakua
na kuchangia maendeleo ya nchi hasa kupitia viwanda.
No comments:
Post a Comment