Wednesday, April 23, 2014

WATOTO WA VIGOGO WAZIDI KUMPIGA VITA LOWASA

Baadhi ya sms ambazo ZIMEVUJA
MKAKATI wa kuzima ndoto za Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa asigombee urais mwaka 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), umevuja, Tanzania Daima Jumatano limedokezwa.
Kwa mujibu wa kielelezo cha waraka wa mawasiliano ya wapinzani wa Lowassa, mkakati huo unaongozwa na mtoto wa kigogo akishirikiana na Umoja wa Vijana (UVCCM) ambao wanadaiwa kumuunga mkono mmoja wa mawaziri wanaotajwa kugombea urais.

Lowassa ni mmoja wa makada wa CCM wanaotajwa kutaka kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais mwaka 2015. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano), Stephen Wassira na William Ngeleja.

Katika mawasiliano yao yaliyovuja na kusambazwa mitandaoni, mtoto huyo wa kigogo na wenzake wanawashambulia kwa maneno makali Hussein Bashe na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kwamba ni vibaraka wanaomdanganya Lowassa kuwa atakuwa rais wa nchi.
Kundi hilo linajitapa kwamba hawawezi kuwapa vichaa nchi wakati uwezo wa kuongoza wanao na kujiapiza kuwa kundi la Lowassa wakiingia Ikulu, wao watahama nchi.
“Ushindi hapa ni Baraza moja kwa moja, ili tujipange mapema. Lazima tuweke majeshi sawa tuweke historia Magogoni (Ikulu). Nilishakwambia mkuu, Lowassa haingii Ikulu.
“Anayemdanganya ni wapambe, wakina Msomali Bashe. Hatutaki walevi Ikulu. Mtu alishakauka hata kutembea hawezi, Ikulu ndio ataweza,” yanasomeka mawasiliano ya kundi hilo ambayo yameambatana na matusi ya nguoni yasiyoandikika kitaaluma.
Katika mawasiliano hayo, anashambuliwa pia January Makamba anayetajwa kuutaka urais, lakini hapa anaelezwa kuwa kibaraka wa Lowassa anayebebwa na Rostam Azizi.
“Hao vijana wa Lowassa wanaelekea kuzimu. Wakiingia Ikulu nahama nchi. Haiwezekani na haitatokea. Halafu huyo mnafiki January ambaye anabebwa na shemeji yake Rostam dawa yake inachemka.
“Muhimu sisi kujipanga, lazima UVCCM iwe imara. Hatuwezi kuwapa vichaa nchi wakati uwezo tunao wa kuongoza. Lazima tujiimarishe ndani na nje ili tushinde 2015,” inasomeka sehemu ya mawasiliano hayo.
Itakumbukwa UVCCM kupitia kwa Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, Paul Makonda na wenzake, wamekuwa wakitumika kumshambulia hadharani Lowassa, wakidai anaharibu chama kwa sababu zake za kusaka urais.
Katika tamko lao la mwisho, vijana hao kupitia Makonda ambaye ni mfuasi wa Membe, mmoja wa wagombea urais watarajiwa kupitia CCM, walidai kuwa Lowassa hana sifa za kuwa rais wala hafai kuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama.
Mkakati huo wa kumshambulia waziwazi Lowassa, ambaye kundi lake limeonekana kuwa tishio ndani ya CCM, ni uthibitisho tosha kwamba siasa za kuchafuana zinazidi kushika kasi wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu 2015.
Licha ya kutoweka wazi msimamo wa kundi analoliunga mkono, Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa mtoto huyo wa kigogo anayemwandama Lowassa kwa kushirikiana na UVCCM anampigania mmoja wa mawaziri ili awe mrithi wa Rais Jakaya Kikwete.
Mkakati huo wa familia ya kigogo kumbeba waziri katika uchaguzi mkuu ujao, ulianzia tangu wakati wa uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka jana, kwa kumpigania apate nafasi hiyo baada ya mambo kuwa yamemwendea vibaya.
Sasa wapinzani hao wa Lowassa wakiongozwa na mtoto huyo wa kigogo, wameanza kutapanya fedha kwa makada wao kwenye kata ili kusimika mizizi ya mtu wao wanayemuunga mkono.
Kupitia mawasiliano yao hayo yaliyofanyika Aprili 5, mwaka huu, mtoto huyo wa kigogo anamwelekeza mwenzake namna ya kuchukua fedha mahala kwa mtu kwa ajili ya kugawia wapambe wao.
“Usisahau kupitia pale Mikocheni kwa … (anatajwa mtu), uchukue milioni 50 uje nazo, ameishazitayarisha. Hakikisheni kila mtu wetu kwenye kata ameachiwa sh milioni 5, anzeni na … (anatajwa mtu mwingine),” yanaonyesha mawasiliano hayo.

CHANZO TANZANIA DAIMA****

No comments:

Post a Comment