Sunday, July 20, 2014

CHADEMA YAZIDI KUPOTEZA WANACHAMA

Picha toka maktaba


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hivi sasa kipo katika mapito magumu ya kujiimarisha yanayoenda sambamba na makada wake kujiengua ndani ya chama hicho kwa madai mbalimbali, ikiwamo hofu ya kuchukuliwa hatua na kupoteza fursa katika uchaguzi wa ndani unaoendelea.
 
Kwa sehemu, sababu ya baadhi yao kujiondoa kwenye chama hicho ni uamuzi mgumu wa Kamati Kuu iliyoketi mwishoni mwa mwaka jana na kuwavua uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Kitila Mkumbo na kumvua nyadhifa zote aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe.

Zitto alifungua kesi Mahakama Kuu, kuzuia CHADEMA kujadili uanachama wake kwa masharti kadhaa.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa baadhi makada wanaojiondoa ndani ya chama hicho wanahofia adhabu kwakuwa tayari wametuhumiwa kwa makosa ya kukisaliti na kushirikiana kukihujumu chama hicho, hivyo wamejiwahi.

Huku baadhi yao, hasa watokao mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi wakiondoka kwa madai ya kukerwa na kile walichoita siasa za ukabila na ukanda, dhana ambayo imekuwa inazungumzwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametangaza kujiunga na chama kipya cha Alliance for Change and Transpatency (ACT- Tanzania) kilichoasisiwa na akina Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, na hivyo kuleta hisia zile zile za ukabila na ukanda wanazodai kupinga kwingine.

ACT- Tanzania inaongozwa na Mwenyekiti wa muda, Kadawi Limbu na Katibu Mkuu Samson Mwigamba.

ACT jana kilipokea wanachama na baadhi ya viongozi kutoka CHADEMA katika Mkoa wa Tabora kikiwa kwenye ziara yake mikoani yenye lengo la kujiimarisha.

Baadhi ya wale wanaong’oka CHADEMA Kigoma wamekuwa wakidai chama hicho kimepoteza mamlaka mkoani humo, lakini bado kinaongoza Halmashauri ya Ujiji.

Tanzania Daima Jumapili, imedokezwa kuwa baadhi ya wafuasi wa Zitto hivi sasa wamekuwa wakiratibu shughuli za kuidhoofisha CHADEMA, ingawa mwenyewe mara kwa mara amekana kuhusika na mipango hiyo.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini, anakotokea Zitto, Ally Kisala, alisema licha ya jitihada za kukisambaratisha chama hicho kitabaki imara zaidi kuliko inavyofikiriwa.

Kauli ya Kisala imekuja siku moja baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa (Bazecha), Jaffari Kasisiko, Katibu wa Mkoa, Msafiri Wamarwa, Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Malunga Masoud na Shaaban Mambo kukihama chama hicho.

Kisala, alisema CHADEMA wamebaini kuwa kuondoka kwa makada wao ni miongoni mwa mikakati ya CCM kukisambaratisha chama hicho kikuu cha upinzani hapa nchini.

Alisema katika kuhakikisha CCM inatimiza kazi hiyo iliwarubuni viongozi hao wazorote/kutofanya shughuli za kukuza chama hicho za kujenga misingi na kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Alisema upo ushahidi wa wazi kwa viongozi hao walioondoka na wenzao waliopangwa kuondoka kwa awamu nyingine, kulalamikiwa kufanya kazi ya chama kingine cha siasa kwa maslahi na maelekezo ya CCM.

“CCM ilihakikisha inafanya kazi zake katika sura mbalimbali ili kuwarubuni viongozi hawa, hivyo kuwa kikwazo kama si kizuizi cha muda mrefu sana kwa chama chetu kustawi na kuwa imara zaidi katika mkoa mzima wa Kigoma.

“Tunaweza kusema kuwa viongozi hawa pamoja na wengine wachache ambao tunajua wako mbioni kuondoka kati ya leo na kesho, walikuwa wanavaa koti linalowabana,” alisema Kisala.

Alisema kuondoka kwa viongozi hao walioshindwa kazi, kumetoa nafasi kwa wanachama wengine kupata uongozi na kufanya shughuli za chama hicho katika kipindi hiki chenye shughuli nyingi za kisiasa.

“Hii ni fursa iliyokuja kwa wakati mwafaka kwa wanachama, makamanda waaminifu na watiifu waliofungiwa milango kwa muda mrefu kuzichukua ili kusonga mbele kukijenga chama chetu kwa imani kubwa ya kuendelea kubeba matumaini ya Watanzania wanyonge,” alisema.

Kisala alisema yalitapakaa maneno ya viongozi hao kuwa wanaondoka kwa sababu ya mbunge wao Zitto kuzuiwa kugombea uenyekiti.

“Sasa tunajiuliza taarifa za nia ya kugombea Zitto ambayo hatujawahi kuisikia ikitangazwa kwa kufuata taratibu za chama, katiba, kanuni, maadili, miongozo na itifaki walizitoa wapi?” alihoji Kisala.

Alitoa wito kwa viongozi wenzake wa wilaya na majimbo ya Kasulu Mashariki, Muhambwe, Buyungu, Kasulu Magharibi, Manyovu, Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini na Kigoma Mjini kukutana kwa ajili ya kikao cha mashauriano kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuimarisha chama chao.

“Katika hali hii ya dharura, tunakiomba chama makao makuu kiingilie kwa kutumia kifungu cha katiba 6.1.3 ili kupata chombo cha kuendelea kuwaunganisha wanachama wakati mkoa ukijiandaa kuchukua hatua hiyo kupitia Baraza la Mashauriano,” alisema Kisala.

Mratibu wa Kanda ya Magharibi, Christopher Nyamwanji, alisema viongozi walioondoka kwenye chama hicho wamefanya hivyo baada ya kuingiwa na hofu ya kushindwa kutekeleza majukumu yao ‘CHADEMA ni msingi’, hivyo wanajua hawezi kuchaguliwa katika chaguzi za ndani za chama.

Kamati Kuu yamaliza kikao
Kamati Kuu ya CHADEMA iliyokutana jijini Dar es Salaam kwa siku mbili – juzi na jana, leo inatarajia kutoa kilichojiri.

Miongoni mwa yaliyojadiliwa ni hali ya kisiasa ikiwemo katiba mpya, uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi wa chama hicho katika ngazi za kitaifa, matatizo ya kijamii na kiuchumi.

Taarifa zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam zilibainisha kuwa leo CHADEMA itakutana na waandishi wa habari kubainisha kilichojadiliwa kwenye vikao vyake vilivyoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.

CHANZO:TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment