Monday, August 25, 2014

Maalim Seif awataka Polisi kutekeleza majukumu kwa kuzingatia maadili

Makamu wa kwanza wa Rais. Maalim Seif Sharif Hamad akiwasalimia maafisa wa Polisi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar 
Makamu wa kwanza wa Rais. Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Polisi Ziwani alipofika kuwatembelea.


Na Khamis Haji, OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa Jeshi la Polisi Zanzibar kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuhakikisha askari hawafanyi kazi kwa misingi ya upendeleo, chuki, rushwa, wala ubaguzi wa aina yoyote.
Maalim Seif ameyasema hayo leo wakati alipotembelea Makao Makuu wa Polisi Zanzibar Ziwani, na kuzungumza na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Makame pamoja na maafisa wa Jeshi hilo.
Makamu wa Kwanza amesema kwa kiasi kikubwa Polisi Zanzibar limepata mafanikio makubwa katika kusimamia majukumu yake, hasa ya kupunguza matendo ya uhalifu, lakini wapo miongoni mwa askari hujihusisha na matendo yaliyo kinyume cha maadili yanayolitia doa jeshi hilo.
Alisema zipo taarifa kwamba baadhi ya Maafisa wa polisi huvujisha taarifa na kuwapa watuhumiwa wa dawa za kulevya, pale jeshi hilo linapojiandaa kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria.

Maalim Seif amesema tabia hiyo haina budi kukomeshwa kwa nguvu zote kwa sababu hudhorotesha mikakati ya kukomesha uingizwaji na biashara ya dawa za kulevya katika visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema dawa za kulevya zinasababisha madhara makubwa kwa wananchi hasa vijana, na Polisi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti uingizwaji wake kwa kushirikiana na taasisi za Kitaifa na Kimataifa.
“Nasikia baadhi ya wakati taarifa huvujishwa na maafisa wa Polisi. Kitengo cha Polizi cha Dawa za Kulevya lazima kiwe na watu waaminifu sana, Kamishna hili ni tatizo kubwa lazima tulikomeshe”, alisema Maalim Seif.   
Amelipongeza Jeshi hilo kwa juhudi kubwa linazozichukua kuwakamata watuhumiwa wa dawa za kulevya na kuwafikisha mbele ya sheria, lakini hata hivyo amesema bado juhudi zaidi zinahitajika kuwamata wafanyabiashara wakubwa ambao mara nyingi hawapatikanwi.
Amesema Jeshi hilo litajipatia sifa kubwa zaidi na kuipatia sifa nchi, iwapo litafanya kazi kwa kuzingatia weledi, ukakamavu na uwezo wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha utawala bora unazingatiwa kikamilifu.
Ameeleza kuwa Polisi wanatakiwa kujiepusha na tabia ya kufanya kazi kwa upendeleo na wahakikishe wanawapatia haki sawa watu wote, iwe kwa viongozi, watoto wa viongozi au wananchi wa kawaida.
“Sisi wanasiasa tuna kawaida jamaa zetu wanapofanya makosa na kukamatwa tunampigia simu Kamishna, msikubali kufanya upendeleo na kuwakandamiza wananchi wanyonge, hakuna mtu aliye juu ya sheria”, alionya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Polisi, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamadan Makame amesema miongoni mwa changamoto zinazolikabili jeshi hilo ni ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi, uhaba wa nyumba za kisasa kwa ajili ya askari, kuibukwa kwa uhalifu mpya wa kwenye mitandao.
Changamoto nyengine amezitaja kuwa kuibuka vikundi vya kidini vilivyosajiliwa na baadhi ya maeneo ya ardhi yanayomilikiwa na Jeshi la Polisi kuvamiwa na viongozi na baadhi ya wananchi.
Aidha, Kamishna huyo amesema ipo haja Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilione Jeshi la Polisi ni lake, licha ya kuwa lipo chini ya Serikali ya Muungano, kwa kurejesha utaratibu wa zamani wa kulisaidia kufanikisha baadhi ya majukumu yake, ikiwemo operesheni maalum zinazotekelezwa hapa Zanzibar.
Hata hivyo, Kamishna Makame alitaja miongoni mwa mafanikio makubwa ya Polisi Zanzibar hivi sasa ni kupungua kwa matukio ya uhalifu mkubwa, kupungua ajali na makosa ya barabarani, wananchi kuongeza imani kwa Jeshi hilo, na kufanikisha vizuri suala la kudumishwa amani katika visiwa vya Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment