Saturday, August 2, 2014
TANZANIA YAJIANDAA KUIKABILI EBOLA
KUENEA kwa ugonjwa wa ebola katika mataifa ya Afrika Magharibi, kumeifanya serikali kuchukua tahadhari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alisema kuwa serikali imeshaanza kazi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Aliwataka wananchi wasiwe na hofu ya ugonjwa huo kwa kuwa wataalamu wa sekta ya afya nchini wanashirikiana na wenzao kukabiliana nao ikiwemo njia za kujikinga.
Mwamwaja alisema wizara yake imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), linalowataka kuchukua tahadhari ya kukabiliana na ugonjwa huo unaoenea kwa kasi.
Alisema hadi hivi sasa ebola haina tiba wala chanjo na Tanzania imeshatoa taarifa ya tahadhari kwa waganga wakuu wote wa mikoa na wilaya.
Kwa sasa ugonjwa huo bado upo mbali na Tanzania, ila kutokana na kasi ya kuenea kwake, wizara imeanza kutenga maeneo maalumu ya dharura iwapo kutatokea mgonjwa.
“Tupo kwenye mikakati ya kuyaweka kinga maeneo yenye kuashiria kupitisha ugonjwa huo kirahisi kama viwanja vya ndege, mikoa inayopakana na nchi jirani kama Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma na Rukwa,” alisema.
Mwamwaja alifafanua kuwa hadi sasa watu 729 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo kwenye nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone na idadi kubwa ya waathirika ikifikia 1,323 tangu kuzuka kwa ugonjwa huo Februari, mwaka huu.
Alizitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na vidonda kooni.
Aliongeza kuwa mara nyingi dalili hizo huambatana na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi huku baadhi ya wagonjwa kutoka damu ndani na nje ya mwili.
SOURCE TANZANIA DAIMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment