Saturday, August 2, 2014
KESI ZA UGAIDI BALAA
KESI za ugaidi jana zilivifanya viunga vya mahakama za miji ya Arusha na Dar es Salaam kutawaliwa na ulinzi mkali wakati watuhumiwa walipofikishwa mahakamani.
Jijini Dar es Salaam, kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed (45) na mwenzake Jamal Swalehe (38) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka manne, likiwemo la ugaidi.
Sheikh Farid na Swalehe walifikishwa mahakamani kwa usiri mkubwa kuepusha vurugu kubwa ingawa kulikuwa na ulinzi.
Idadi kubwa ya waandishi waliokuwa Mahakama ya Kisutu walifichwa uwepo wa kesi hiyo hadi watuhumiwa hao walipokuwa wakiondolewa eneo la tukio baada ya kusomewa mashitaka yao.
Kiongozi huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, na Mwendesha Mashitaka Peter Njike akidaiwa kujihusisha na matukio ya kigaidi kati ya Januari 2013 na Juni 2014 katika maeneo mbalimbali nchini.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao walipanga na kula njama ya kuwaagiza watu kufanya vitendo vya ugaidi.
Njike alidai kuwa shitaka la tatu na nne yanayomkabili Sheikh Farid ni mnamo Januari 2013 na Juni 2014 aliwaagiza Farah Omary na Sadick Absalom kufanya vitendo vya ugaidi.
Katika shitaka jingine, Sheikh Farid, anadaiwa kuwasaidia watu hao kufanya vitendo vya ugaidi.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na wamerudishwa rumande ambapo kesi yao itatajwa tena Agosti 6, mwaka huu.
Mkoani Arusha
Watu 19 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa mashitaka 30 tofauti ya mauaji, kujaribu kuua, kula njama na kufanya vitendo vya kigaidi na kufadhili kufanyika kwa matendo ya kigaidi.
Makosa mengine ni kusambaza zana za ugaidi, kushawishi na kufadhili watu kujiunga na kundi la kigaidi la Al Shabaab.
Watu hao wanahusishwa na matukio ya mabomu kwenye mkutano wa CHADEMA, milipuko kwenye nyumba za masheikh, Abdulkarim Jonjo na Sudi Ally Sudi na kuwamwagia tindikali Mustafa Kiago, Halidi Mustafa kwenye msikiti mkuu wa Ijumaa na Sheikh Saidi Mkamba.
Watu hao walisomewa mashitaka yao jana na waendesha mashitaka wa serikali, Agustino Kombe, Felix Kwelukira na Marselino Mwamunyange mbele ya hakimu mkazi, Devote Msofe.
Washitakiwa 12 walisomewa shitaka la kula njama na kufanya vitendo vya kigaidi kinyume na sheria ambapo ilidaiwa kati ya Januari na Februari mwaka huu walikula njama na kufanya matendo ya kigaidi.
SOURCE TANZANIA DAIMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment