Saturday, August 2, 2014
UKAWA WAKWEPA MTEGO WA CCM
KITENDAWILI cha iwapo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) watarejea bungeni jana kilishindwa kuteguliwa baada ya mkutano wa mwisho wa kutafuta maridhiano kukwama.
Kikao hicho kilichoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi, kilitawaliwa na mivutano mikali baina ya wajumbe wa UKAWA na wale kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Tanzania Daima, kikao hicho kilianza kwa mkwamo baada ya wajumbe wa CCM kugoma kuanza kikao wakilenga UKAWA wasitumie umoja huo bali wajitambulishe kwa vyama vyao.
Hujuma za CCM kutaka kuwagawa wajumbe wa UKAWA zilionekana kugonga mwamba baada ya umoja huo kugomea hila hizo.
Hali hiyo ilikifanya kikao hicho kiahirishwe kwa muda kupisha majadiliano ya viongozi wakuu wa UKAWA unaoundwa na wajumbe kutoka vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF kuteta na baadae kurejea na kukataa sharti hilo.
Kikao hicho cha jana kilikuwa ni cha mwisho kabla ya wabunge wa Bunge Maalum kuanza vikao vyake Agosti 5 mjini Dodoma.
Katika mfululizo wa vikao hivyo vya maridhiano, cha kwanza kilichofanyika wiki moja iliyopita kilimalizika bila kupatikana muafaka.
Katika kikao cha jana, inadaiwa wajumbe wanaotokana na UKAWA walipinga kwa nguvu zote mkakati huo wa kuwagawa na kueleza kwamba, walipotoka katika Bunge Maalum la Katiba, walikuwa na umoja wao na kueleza kuwa kuwatenganisha kivyama katika maridhiano hayo ni mkakati wa makusudi wa kutaka kuwagawanya ili kupenyezwe ajenda zinazowafurahisha wana CCM.
Mabishano hayo yanadaiwa kusababisha mkutano huo wa maridhiano kuahirishwa kwa muda na wajumbe kupata muda wa kupumzika kabla ya kurejea tena, huku ajenda ya kutaka kuwatenganisha UKAWA ikiwa imetupwa pembeni.
Hata hivyo, waandishi wa habari hawakuweza kupata ajenda zilizojadiliwa katika kikao na uamuzi uliofikiwa, huku Jaji Mutungi, akitaka ahojiwe yeye juu ya kilichojiri.
Hata hivyo, Jaji Mutungi, alisema kilichozungumzwa kwenye kikao hicho atakiweka wazi leo kwa waandishi wa habari.
Mbali na Jaji Mutungi, pia taarifa zinaeleza kuwa Baraza la Vyama vya Siasa, nalo litakutana kwa ajili ya kujadili yaliyojitokeza katika mkutano wa jana.
Juzi wakati wenyeviti wa vyama vinavyounda UKAWA walipozungumza na waandishi wa habari, walisema msimamo wao ni kutohudhuria vikao vya Bunge hilo kama matakwa yao hayatatimizwa.
Katika mkutano huo wa juzi, Freeman Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA, alisema wataridhia kurudi bungeni, endapo mjadala mzima utajikita kwenye rasimu ya katiba, ambayo imebeba mapendekezo ya wananchi na kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka CCM, kuacha kujenga hoja kwa kutumia kejeli, matusi na mizaha.
Aprili 16, mwaka huu, UKAWA walisusia vikao vya Bunge hilo la katiba, wakipinga kubadilishwa rasimu ya katiba na wajumbe wa CCM, kwa maelezo kuwa ni kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
UKAWA walidai vikao vya Bunge Maalum vilikuwa vikiendeshwa kwa ubaguzi, matusi, kejeli na kutofuata rasimu iliyowasilishwa na Tume.
source TANZANIA DAIMA .. Sauti ya Watu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment