Kisa:Walichelewa nyumbani kutoka kuangalia tv
Watoto
wanaodaiwa kufanyiwa ukatili wakionyesha vidonda kwenye mikono yao
ambavyo vinatokana na kuchomwa moto na baba ya mzazi nyumbani kwao
Mbagala Kibondemaji jijini Dar es Salaam jana.
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
vinavyofanywa na baadhi ya wazazi, vimezidi kukithiri nchini baada ya
watoto wawili kudaiwa kuchomwa moto mikono na baba yao kwa kutumia tambi
za jiko jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, anayetuhumiwa kufanya
unyama huo ni Salum Juma, fundi gereji wilayani Temeke, mkazi wa Mbagala
Kibonde Maji, jijini Dar es Salaam.
Watoto hao mmoja mwenye umri miaka
saba na mwingine miaka mitano (majina yao yamehifadhiwa), akiwamo wa
kumzaa na wa kufikia walikutwa na mkasa huo baada ya kwenda kuangalia
runinga kwa jirani na kurudi nyumbani saa 5:00 usiku Alhamisi wiki
iliyopita.
Akizungumza na NIPASHE, jirani yao,
Omar Fusi, alidai watoto hao walieleza kuwa walichomwa na baba yao na
kufichwa ndani, lakini baadaye majirani waliwaona watoto hao wakiwa na
majeraha.
Fusi alisema baada ya kuwaona wakiwa
na majeraha, waliwahoji ambapo walieleza kuwa walichomwa na baba yao
baada ya kuchelewa kurudi kutoka kuangalia televisheni.
Kwa mujibu wa Fusi, kitendo hicho kilifanyika huku mama yao akiwa kwenye biashara zake za kukaanga mihogo.
Fusi alisema baada ya kubaini tukio
hilo alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibonde Maji
‘B’, Teofile Balae, ambaye alitoa taarifa kwa Ofisa Ustawi wa Jamii kata
ya Mbagala, Eliameresa Kaaya na kuripoti polisi na kufanikisha baba
huyo kukamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Maturubai ambako
anaendelea kushikiliwa.
Balae alisema baada ya kushirikiana
na Ofisa Ustawi wa Jamii na baba huyo kukamatwa, waliwachukua watoto hao
na kuwapeleka Kituo cha Polisi Mbagala Kuu kwa ajili ya kupata fomu ya
PF3 na kuwapeleka katika hospitali ya Mbagala Rangi Tatu kupatiwa
matibabu.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Erasto
Kibara, alisema walibaini watoto hao kufanyiwa ukatili huo baada ya
kumkuta mmoja wao adukani alikotumwa akiwa na majeraha na kumuuliza
kilichompata kisha alitoa taarifa hizo kwa mwenyekiti wa mtaa huo.
Ofisa Ustawi wa Jamii, Kaaya,
akizungumza na NIPASHE katika Kituo cha Polisi Maturubai wakati watoto
hao wakichukuliwa maelezo na polisi, alisema kitendo walichofanyiwa
watoto hao ni cha kikatili na kuwataka wananchi kutoa taarifa pale
wanapogundua ukatili katika mitaa yao ili kutokomeza vitendo hivyo
vilivyoshika kasi nchini.
NIPASHE iliwashuhudia watoto hao
katika Kituo cha Polisi Maturubai huku wakiwa na majeraha mkononi wakati
wakichukuliwa maelezo na maofisa wa polisi wa kituo hicho.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya
Mbagala Rangi Tatu, Dk. Julius Nyakazilibe, alithibitisha watoto hao
kupokelewa hospitalini hapo na kupatiwa huduma ya matibabu kutokana na
majeraha yaliyosababishwa na moto.
“Ni kweli watoto hao tuliwapokea hapa
hospitalini wakiwa na Ofisa Ustawi wa Jamii na walipatiwa matibabu,”
alisema Dk. Nyakazilibe. Mama mzazi wa watoto hao, Christina Menasi,
akiwa katika kituo cha polisi na mtoto wake mchanga huku akimnywesha
uji, alisema wakati wa tukio hilo, alikuwa katika biashara yake ya
kuchoma mihogo na aliporudi nyumbani na kukuta hali hiyo, aliingiwa na
hofu ya kuripoti tukio hilo kwa kumhofia mumewe.
Mama huyo alilaani kitendo hicho cha kikatili lakini alisema akifungwa yeye ndiye atakuwa na mzigo mkubwa wa kulea familia hiyo.
“Inatakiwa tuache vitendo hivi vya
kikatili, lakini ikiwa mume wangu atafungwa, mimi ndiye nitakayebeba
mzigo wa kulea hii familia,” alisema Christina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke,
Kihenya Kihenya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa
mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Maturubai na kwamba
upelelezi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue
mkondo wake.
mmh Mungu atusaidie
ReplyDelete