10612541_635931856514532_1179852893165923510_n
Mjumbe wa Kamati ya utendaji MISA -TAN, Lilian Lucas Kasenene akimpongeza Mwenyekiti  mpya wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Simon Berege.
Na Nathaniel Limu
Mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama cha waandishi wa habari kusini mwa Afrika (MISA-TANZANIA), umemchagua kwa kishindo Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Iringa, Simon Berege kuwa mwenyekiti wake kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.Berege ambaye alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, alizoa kura zote 26 za ndio zilizopigwa.Ushindi huo ni wa asilimia mia moja wa kura zote zilizopigwa na wajumbe wa mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa makao makuu ya MISA-TAN uliopo Mkwajuni Mwananyamala jijini Dar-es-salaam.

Mhadhiri huyo ambaye pia ana taaluma ya uandishi wa habari,amechukua nafasi hiyo iliyokuwa inashikiliwa na Mwanasheria Mohammed Tibanyendera, aliyemaliza muda wake.
Mwenyekiti wa mkutano huo wa uchaguzi,Tibanyendera,aliwatangaza Liliani Lucas Kasenene na Abdala Mohammed Mmanga kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji, baada ya kupata kura 23 (za Liliani) na 17 (za Mmanga).Mgombea mwingine wa nafasi hiyo,Timoth Kitundu,aliambulia kura nane.
Tibanyendera alisema nafasi za makamu mwenyekiti na ile ya mweka hazina,zitatangazwa baadaye kutokana na kukosekana na wagombea katika nafasi hizo, licha ya kutangazwa sana.
Akiwashukuru wapiga kura wake, Mwenyekiti mteule Barege, alisema ushindi wa asilimia mia moja ,hauwezi kusababisha yeye abweteke na badala yake utakuwa chachu kwake ya kuchapa kazi kwa bidii na maarifa ili kukidhi matarajio ya wapiga kura wake.
Katika hatua nyingine ,taarifa ya fedha ya MISA-TAN kwa mwaka jana, imebainisha kuwa taasisi hiyo inadaiwa zaidi ya shilingi 124.3 milioni na wadau mbalimbali.
Ilidaiwa kwamba mamlaka ya mapato Tanzania (TRA),inadai zaidi ya shilingi 93.1 milioni, mkaguzi wa mahesabu 1.6 milioni na mfuko wa NSSF,2.9 milioni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,taasisi hiyo imekusanya mapato ya zaidi ya shilingi 141.2 milioni kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya mapato kwa kipindi cha mwaka jana,kati ya matarajio ya kukusanya zaidi ya shilingi 322.9 milioni iliyotatajia kukusanya.